Home || The Aggressive Vision || Prophetic Word Of The Lord || On Line Library || Current Articles and What's New
Free Literature || Visions from The Lord || More About ACMTC || Contact


Inamaanisha Nini Kuwa Umepotea (What it Means to Be Lost)

Kumbuka: neno “Kanisa” katika Agano Jipya linapatikana mara 79 katika tafsiri ya Biblia iitwayo toleo la King James. Neno hili ni la Kiyunani liitwalo Eklessia. (Strong's # G1577, ἐκκλησία). Linamaanisha “walioitwa kutoka” “jamii ya Kikristo” halihusu “kanisa” kama tuliyonayo leo ambapo kila mtu anaishi peke yake, kila mmoja kwake akifanya mambo yake na kukutana pamoja mara chache katika wiki na kufanya ibada. Bali humaanisha muunganiko hasa wa mwili kwa wale waliowaamini halisi wa KRISTO waliojitenga na dunia, wakazama na kujiweka wakfu kutimiza Mapenzi ya Kristo.

HALI YA KUPOTEA ya ubinadamu wote nje ya Yesu Kristo ndio kauli ya ushuhuda wa Agano Jipya. Ukweli huu wa kutisha hauwezi kupingwa na wale wanaoupokea ushuhuda wa Maandiko kama ulio na mamlaka na ulio halisi, kwa habari ya imani ya mwanadamu na katika utendaji. Kwa hakika kuna aina mbili tu za watu: waliookolewa na waliopotea. Na, kila mtu lazima aangukie kwenye kundi moja au jingine. Katika makundi haya hakuna cha kuwa katikati au nusu sehemu.

     Mtu wa asili hurudi nyuma inapofikia kufikiria hali yake ya kupotea. Anagundua kuwa hayuko kamili, yuko mbali sana, bado hawezi kuwaza kwamba hali hiyo inampeleka upotevuni. Anahisi kwamba lazima kuwepo na kitu ndani yake, au kitu Fulani anatakiwa kufanya kitakachomweka mikononi mwa Mungu kitakachomfanya apate upendeleo machoni mwa Mungu. Mungu hajakosa huruma kiasi cha kumtupa moja kwa moja. ANAHITIMISHA HIVYO. Watu wanaoishi kwa kuyashika maadili kwa kiwango cha wastani huwa wagumu kupokea ukweli wa maandiko wakijiona wako sawa hadi pale Roho wa Mungu atakapofanya kazi ya ushawishi ndani yao.

     Biblia ndicho chanzo cha kutegemewa cha maarifa kwa mantiki hii. Falsafa, miiko, makabila na dini zisizo za Kibiblia hazina mafunuo, na hivyo, huwa na tabia ya humtukuza mwanadamu badala ya kumhukumu. Ufahamu na maoni ya wanadamu sio vitu vya kuaminika kwa mtu akiwa kiumbe mdhambi ana MOYO ULIOPOTOKA NA NIA ZILIZOFUNGA GIZA. HAWEZI KUJIUNDIA HUKUMU ILIYO SAHIHI JUU YA NAFSI YAKE ACHILIA MAFUNUO YA KIMBINGU.

     Mpango halisi wa ki-Biblia wa wokovu upo kwenye uaminifu na uhalisi wa upotevu wa mwanadamu. Lazima tukubali mafundisho ya Biblia hapa au tuachane nayo yote. Lazima tuupe uzito ushuhuda huu kwa makini.

     Agano Jipya linafunua kwamba dhambi za wanadamu zaweza kuwa katika utofauti mpana kwa kiwango zilivyofanywa lakini hakuna utofauti wa kiwango cha dhambi cha kumtenga mtu na Mungu. Wengine wametenda dhambi nyingi kuliko wengine lakini haijalishi wote ni wadhambi na wadhambi wote wamepotea. Wadhambi WAMEPOTEA KABISA SIO KWAMBA WAMEPOTEA KWA SEHEMU. Wamepotea sasa - labda watubu na kumwamini Yesu Kristo. Hawahitaji kusubiri hadi matendo yao yachunguzwe na kupimwa mbele ya hukumu ya Mungu ili kujua hatima ya umilele wao. Hayo yote hukusudiwa hapa tena sasa, kwa namna ya mwelekeo wa uhusiano na Mwana wa Mungu.

     Wakristo hawataweza kuwa na uzoefu wa huruma ya wokovu kwa roho zinazopotea hadi pale mafundisho ya Biblia yatakapozama kwa wingi ndani ya mioyo yao. Ni lazima waijue hali ya watu wakukata tamaa kabla hawajajaribu kuwavuta kwa Kristo.

     Vifungu vikubwa zaidi katika Biblia vinavyohusu kupotea ni; Rumi 3:9-20; Efeso 2, na Yohana 3. Tukianza na vifungu hivi na tukiorodhesha vipengele tofautitofauti tunapata kwa uchache nia mia moja ambazo Agano Jipya linaelezea hali ya mwanadamu ya kupotea. Tukifuatilia toleo la Biblia la American Standard tutapata orodha ya mashtaka yaliyoandikwa.

Rumi 3:9-20 inazungumzia juu ya watu wote, Wayahudi na Wayunani;

1.  Wote wako chini ya dhambi (mst. 9)

2.  Hakuna mwenye haki, hayupo hata mmoja, (mst.10)

3.  Hakuna afahamuye (mst.11)

4.   Hakuna amtafutaye Mungu (mst.11)

5.   Wote wamepotoka (mst.12)

6.   Wameoza wote pia (mst 12)

7.  Hakuna mtenda mema la, hata mmoja (mst 12)

8.    Koo lao ni kaburi wazi, kwa ndimi zao wametumia hila, sumu ya fira i chini ya midomo yao (mst 13)

9.    Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu (mst 14)

10.Miguu yao ina mbio kumwaga damu (mst 15)

11.  Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao (mst 16)

12.Wala njia ya amani hawakuijua (mst 17)

13.  Kumcha Mungu hakupo machoni pao. (mst 18)

14.Kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu (mst 19)

15.  Kwa maana hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria (mst 20)

     Mashtaka haya yaliyoandaliwa kwa ulimwengu wote yamechunguzwa kwa makini. Mengi ya haya yametajwa pia kwenye kitabu cha Zaburi, mojawapo ya kitabu kinachopendwa sana cha Agano la Kale. KILA SHARTI NA DHAMBI ZILIZOTAJWA HAPA NI HALISI KWA KILA MTU AMBAYE HAJAOKOKA, AIDHA KWA HALISIA AU INAYOWEZEKANA KUWA.

     Mtu mmoja alipendekeza namna ya kukitumia kifungu hiki kipekee katika kushughulika na wasiookoka kuwaleta katika kuwafanya washawishike. Mtu akikataa matumizi ya fungu hili katika nafsi yake, mwambie asome fungu hili kwa sauti ila aweke maneno haya “isipokuwa mimi” kila baada ya kifungu. Kwahiyo asome hivi:

“…..wote wako chini ya dhambi isipokuwa mimi kama ilivyoandikwa Hakuna mwenye haki, hakuna, hayupo hata mmoja, isipokuwa mimi: Hakuna anayeelewa isipokuwa mimi….”

     Tafsiri ya namna hii itamthibitishia kuwa YEYE SIO MTU WA PEKEE. Kwamba hakuna atakayethubutu kujiona hana hatia katika mashitaka yaliyoko kwenye fungu hili. Maandiko hayajakusudiwa [kumtoa] mtu yeyote.

     Waefeso 2 ni kifungu kingine muhimu kinachohusu kipimo cha Mungu kwa wale walioko nje ya Yesu Kristo. Sura hii inazungumza na wale waliookolewa na inafunua kile nguvu ya enzi ya Mungu ilichofanya kuwakomboa kutoka katika hofu ya kale. Vipengele vyote kwenye sura hii pia vinahusika kama ilivyo uzoefu wa wakati huu kwa watu wote ambao hawajaokoka, hasa Wapagani.

16 Ni wafu kwa sababu ya makosa na dhambi (mst. 1,5)

17 Ambazo mlizitenda zamani kwa kuifuata kawaida ya Ulimwengu huu. (mst. 2)

18 Kwa kumfuata mfalme wa uweza wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa uasi. (mst. 2)

19. Ambao zamani, sisi sote nasi tulienemda kati yao, katika tama za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia. (mst. 3)

20. Tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. (mst.3)

21. Tulikuwa hatuna Kristo (Mst.12)

22. Tumefarakana na jamii ya Israeli (mst.12)

23. Tulikuwa wageni wasio na maagano ya ahadi ile (mst.12)

24. Tulikuwa hatuna tumaini, hatuna Mungu duniani. (mst.12)

25. Tulikuwa mbali hapo kwanza (mst. 13)

     Fungu la tatu ambalo ni kubwa zaidi linalohusu waliopotea ni lile linalofahamika vizuri lililopo kwenye sura ya tatu ya Injili ya Yohana. Kama hizi kweli zilifanya kazi kwa Nicodemo, Farisayo mshika dini wa daraja la juu, basi lazima zifanye kazi na kwa watu wote wasiookoka. Hebu tuviongeze vifungu hivi katika vile ambavyo tumeshaorodhesha:

26. Wote lazima wazaliwe mara ya pili, vinginevyo hawawezi kuuona ufalme wa Mungu. (Mst.3)

27. Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu (mst.5)

28. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili na ni lazima mtu azaliwe katika Roho (mist.6, 7)

29. Mtu wa mwilini hawezi kuzielewa kweli hizi za Roho (Mist 9, 12)

30. Wale wasioamini wanapotea (mst. 16)

31. Asiyemwamini amekwisha kuhukumiwa kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. (mst. 18)

32. Waliopotea wanapenda giza kuliko nuru kwa maana matendo yao ni maovu. (mst19)

33. Kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. (mst.20)

34. Asiyemwamini Mwana hataona uzima. (mst.36)

35. Ghadhabu ya Mungu inamkalia yule anayemkataa Mwana wa Mungu. (Mst.36)

     Tunakubali kwamba baadhi ya vipengele vilivyoorodheshwa vinawiana na vingine kiasi kwamba vingeweza kuchanganywa pamoja ili kupunguza wingi wa vipengele, lakini lengo letu ni kuonesha vifungu tofauti katika Agano Jipya vinavyosisitiza ukweli wa hali ya kupotea kwa mwannadamu. Lakini tumefafanua tu vyema kwa kutilia maanani mchanganuo wa Mungu kwa kile kilicho kibaya kwa binadamu.

     Kifungu kingine ni 2 Timotheo 3:1-9, kinahusu nyakati za hatari za siku za mwisho. Tunaongeza vifungu hivi kwenye vile vingine:

36. Watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe. (mst.2)

37. Wenye kupenda fedha (mst 2)

38. Wenye kujisifu (mst. 2)

39. Wenye kiburi (mst. 2)

40. Wenye kutukana (mst. 2)

41. Wasiotii wazazi wao (mst. 2)

42. Wasio na shukrani (mst. 2)

43. Wasio safi (mst. 2)

44. Wasio wapenda wa kwao. (mst.3)

45. Wasiotaka kufanya suluhu. (mst.3)

46. Wasingiziaji. (mst.3)

47. Wasiojizuia (mst.3)

48. Wakali. (mst.3)

49. Wasiopenda mema. (mst.3)

50. Wasaliti (mst.4)

51. Wakaidi (mst.4)

52. Wenye kujivuna. (mst.4)

53. Wapendao anasa kuliko kumpenda MUNGU. (mst.4)

54. Wenye mfano wa utauwa lakini wakizikana nguvu zake (mst.5)

55. Wanaojiingiza kwenye nyumba za watu na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tama ya namna nyingi. (mst.6)

56. Wakijifunza siku zote ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli (mst.7)

57. Wanaopingana na ile kweli ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani. (mst,8)

     Orodha hii ya mwisho ya dhambi, ni zile ambazo ‘watu’ (kwa kiyunani anthropoi), matabaka ya wanadamu huzifanya. Labda Paulo hakumaanisha kufundisha kwamba kila mtu asiyeokoka atakuwa amezitenda zote, kwani hiyo haionekani kuwa ndio kiini. LAKINI DHAMBI ZOTE HIZI ZIKO KWENYE MPANGILIO MMOJA WA DHAMBI ZINAZOTIRIRIKA KUTOKA KATIKA UTU WA KALE. ZOTE HIZI HATA KAMA HAZIFANYIKI ZIMO NDANI YA KILA MTU ASIYEOKOKA [ na hata waliookoka]. na hakuna yeyote anayeweza kueleza atafanya ngapi kabla uhai wake haujamalizika. Wakati tunapotafakari kwamba kuwaza (kufanya dhambi) ni njia moja ya kuitenda ile dhambi (Mat. 5:28), haiwezi kuwa ngumu kuamini kwamba asiyeokoka ana hatia ya kuzitenda hizi zote. Kama matendo yote haya ya dhambi yanajenga hisia ya kwamba ukitenda mojawapo umefanya zote, basi hakuna shaka kwamba watu wote wanahatia ya kuzitenda zote. (ona Yak.2:10). Hakika dhambi zote kwenye mpangilio huu hufanya kila siku, mara mamia katika majiji haya ya kisasa.

Katika Marko 7:21-23 Yesu anatoa orodha ya dhambi zinazotoka ndani ya mioyo ya wanadamu;

58. Mawazo mabaya (mst.21)

59. Uasherati (mst.21)

60. Wivi (mst.22)

61. Uuaji (mst.22)

62. Uzinzi (mst.22)

63. Tamaa mbaya (mst.22)

64. Ukorofi (mst.22)

65. Hila (mst.22)

66. Ufisadi (mst.22)

67. Kijicho (mst.22)

68. Matukano (mst.22)

69. Kiburi (mst.22)

70. Upumbavu (mst.22). “Haya yote yalito maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu” unajisi. (mst.23)

     Hali kadhalika, twaweza kusema juu ya hizi dhambi kwamba ijapokuwa hazionekani wazi kwa kila asiyeokoka, bado inawezekana zimo, na kuzihifadhi katika nia ni sawa na kuzitenda.

Kweli nyingine katika Agano Jipya kuhusu wasiookoka zinakamilisha orodha hii ifikie mia moja.

71. Wanapitia mlango mpana uendao upotevuni. (Mat. 7:13).

72. Wako kinyume na Yesu kwakuwa hawako pamoja nae. (Mat. 12:30; Luka 11:23).

73. Wamepotea (Luka 15:24, 32; 19:10; Mat. 10:6; 2 Wakor. 4:4).

74. Hawawezi kumwabudu Mungu inavyotakiwa. (Yoh. 4:22-24; 14:6; 5:22-23; 8:42; Mdo 17:23).

75. Hawamheshimu Baba kwa kuwa hawakumheshimu Mwana. (Yoh. 5:22-23)

76. Ni wa Ulimwengu; wale wanaomchukia KRISTO. (Yoh. 7:7; 15:19; 1 Wakor. 2:8).

77. Hawawezi kwenda pale Kristo alipo. (Yoh. 7:34; 8:21).

78. Ni watumishi (watumwa) wa dhambi (Yoh.8:34)

79. Ni watoto wa ibilisi. (Yoh 8:42-47; 1 Yoh. 3:10).

80. Ni maadui wa Mungu. (Rum. 5:10; 8:7).

81. Ni wa kizazi kikaidi (Mdo 2:40).

82. Wako gizani, na chini ya nguvu ya shetani (Mdo 26:18; Efe. 2:2).

83. Wako chini ya ghadhabu ya MUNGU iliyodhihirishwa kutoka Mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu. (Rum. 1:18).

84. Hawawezi kumpendeza MUNGU. (Rum. 8:8; Waeb. 11:6).

85. Kila walifanyalo ni la dhambi kwa kuwa hayatokani na imani (Rum.14:23; Waeb. 11:6).

86. Vitu vya Mungu ni upumbavu kwao (1 Wakor. 2:14; 3:19).

87. Injili imesitirika kwao kwa kuwa mungu wa dunia hii (Shetani) ameyapofusha fikra zao (2 Wakor 4:3-4)

88. Hawajavaa vazi la harusi na kwahiyo watatupwa nje (Mat. 22:11-13).

89. Wanaacha kuyatenda mema wanayotakiwa kutenda na kwao hiyo inakuwa dhambi (Yak. 4:17).

90. Hawana udhuru kwa dhambi wazitendazo (Yoh 15:22; Warumi. 1:20; 2:1).

91. Hawafahamu na huduma ya baraka ya Roho Mtakatifu. (Yoh 14:17, 26; 16:13, 14).

92. Mara zote humpinga Roho Mtakatifu (Mdo 7:51; 28:27; Yoh 16:8-11).

93. Wanashupaza mioyo yao na kujiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira ya hukumu ya Mungu (Rum. 2:5; Waeb. 10:29).

94. Wametawaliwa na asili ya udhalimu ambayo huzaa matendo kumi na tano ya mwili: “Uasherati, uchafu,ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina ,faraka, uzushi,husuda ulevi, ulafi na mambo yanayofanana na hayo. Watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu” (Wagal. 5:19-21; cf. 1 Wakor. 6:9-11).

95. Paulo angewaelezea kama wasiokuwa na akili, waasi, waliodanganywa, wanaotumikia tamaa na anasa za namna nyingi, wanaoishi katika uovu na husuda, wanaochukiza na kuchukiana, (Tito 3:3).

96. Watakufa katika uovu wao wasipompokea Yesu Kristo. (Yoh 8:24). Kila mtu atakufa aidha kwenye dhambi zake au katika Kristo.

97. Wako kwenye hatari ya maangamizo, muda wote waishipo bila Yesu. (Mdo 3:23, 1 Wathes. 5:3; 2 Wathes. 1:9).

98. Wanaelekea kuupata mshahara wa dhambi, ambao ni mauti : ya mwili, nafsi, roho na milele. (Rum. 6:23).

99. Bwana Yesu atawalipiza kisasi wale wasiomjua Mungu wakati atakapofunuliwa toka mbinguni na Malaika wake wakuu kwa vile hawakumjua Mungu na hawakuitii injili. (2 Wathes. 1:7-8).

100. Watasimama katika hukumu mbele ya kiti kikuu cha enzi na kuhukumiwa sawa na yale yaliyoandikwa kwenye vitabu sawa na matendo yao. Matokea yake watatupwa katika ziwa la moto kwa milele yote, ambayo ndiyo mauti ya pili. (Uf. 20:11-15).

Vipengele vyote hivi vinahusiana na wewe. Kwa halisi, au, uwezekano wa kuhusika upo.

Sio mambo ya kufikirika yasiofaa yatokanayo na mawazo yasiyofaa wala sio ubunifu wa kutisha wa wasomi wa mambo ya kale. Hapana mara elfu. NI TAARIFA ZA BUSARA ZA NENO LA MUNGU LENYE UZIMA AMBALO LINAISHI NA KUDUMU MILELE.

Tumetoa maelezo haya kwenye orodha iliyofikia mia moja sio kwa sababu hiyo ndio namba kamili katika Agano Jipya. Hapana ingeweza kufanywa ndefu zaidi. Tumejaribu kuifanya ya kuvutia – tunatamani kufunua wazi na kwa nguvu zote asili, hali, mwenendo, hatari na umilele wa wasiookoka, wanahitaji kujua na marafiki na ndugu zao wanahitaji kujua jinsi wanavyosimama mbele ya macho ya Mungu. Kupotea inamaanisha nini? HAKUNA dhamira ya mtu yenye uwezo wa kufahamu kwa ukamilifu ila Mungu anajua na amejaribu kutupatia habari kwamba inamaanisha nini kupitia vipenngele hivi mbalimbali vya Agano Jipya.

Hebu tusidanganyike wala kujiliwaza kwa kutegemea mtizamo wa nje wa falsafa zilizotengenezwa na wanadamu na za kidini. Kwa masihara na mizaha ya kidunia na uongo wa shetani. Waliopotea wametuzunguka. Hatari yao ni kuu kuliko kaburi, hebu tuamini hivyo! ‘Wakristo’ wamepungukiwa na uwajibikaji, mzigo, huruma na nguvu ya maombi – kupotea kwa watu kumeonekana kana kwamba ni jambo jepesi. Hebu Bwana kupitia neno lake na kwa Roho Mtakatifu atuamshe tuelekee kwenye kweli yake, ILI TUWEZE KUISHI NA KUFANYA KAZI, YA KUTAFUTA NA KUWAOKOA WALE WALIOPOTEA SASA.

 

 

Tungependa kusikia kutoka kwako!

Kuagiza machapisho au taarifa nyinginezo

zinazotuhusu sisi au jamii yetu tafadhali

WASILIANA NASI

 

 


Kwa maelezo zaidi kuhusu ACMTC TANZANIA, au jinsi utakavyoweza kujihusisha, wasiliana na Meja Frank & Elina Materu: S.L.P. 7579 Dar es Salaam, Tanzania. Barua pepe: materufrank@yahoo.com